Polisi nchini Misri, wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya
waandamanaji wanaomuunga mkono rais aliyeondolewa mamlakani Mohammed Morsi
wakati wa maandamano yao mjini Cairo.
Vikosi vya usalama
viliingilia maandamano hayo baada ya wafuasi wa Morsi kukabiliana na mahasimu
wao wa kisiasa.
Walioshuhudia
vurugu hizo walirushiana mawe na chupa huku watoto na wanawake wakikimbilia
usalama wao.
Morsi aliondolewa
madarakani na viongozi wa jeshi mwezi Julai kufuatia maandamano makubwa sana.
Tangu hapo jeshi
limeweka serikali ya mpito.
Wafuasi wa Morsi
aliyeingia madarakani baada ya vuguvugu la kiisilamu la Brotherhood kushinda
uchaguzi wa rais, wanakataa kukubali serikali mpya ya mpito wakisisitiza kuwa
lazima rais wao arejeshwe mamlakani.
Vurugu za Jumanne
zilianza wakati wafuasi wa Morsi, walipotembea hadi sehemu moja ya Cairo ambako
watu wengi wanapinga vuguvugu la Muslim Brotherhood.
Waandamanaji hao
walijaribu kuingia katika ofisi za wizara moja ingawa polisi waliwalazimisha
kuondoka kwa nguvu.
Wakaazi wa eneo
hilo walianza kuwakejeli waandamanaji na hapo ndipo polisi walipoingilia mzozo
huo.
Mamilioni ya
wamisri waliandamana kumtaka Morsi aondolewe mamlakani ingawa wadadisi wanasema
kuwa kuondolewa kwake kunaonekana kuzorotesha migawanyiko ya kisiasa iliyoko
kwa sasa.
Wafuasi wake
wamekuwa wakipiga kambi mjini Cairo wakitaka arejeshwe mamlakani.
Maafisa wa usalama
walitishia kuondoa mahema waliyoweka wafuasi wa Morsi ambako wamekuwa wakipiga
kambi lakini wakabatili uamuzi wao baada ya kuamua kuuakhirisha.